Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekanusha taarifa kuwa mradi wa Umeme Vijijini  unaoratibiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ulikuwa ukiwezeshwa na fedha za Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) la Marekani.

Akimjibu Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa katika kikao cha Bunge leo, Muhongo amesisitiza kuwa mradi huo haukutumia hata senti moja ya MCC.

“Hakuna hata senti moja ya MCC iliyokuwa kwenye mradi wa umeme vijijini,” alisema Muhongo. “Na hiyo hauwezi kunibishia ndugu Msigwa kwa sababu mimi mwenyewe ndio nimeenda kukaa na watu wa MCC, nimekaa na waziri wa nishati na Waziri wa fedha wa Marekani. Hizo fedha zilikuwa haziji Bungeni hapa,” aliongeza

Aidha, alieleza kuwa fedha za MCC sio zote zilizokuwa zikielekezwa kwenye mradi wa kuunganisha umeme vijijini kwani kulikuwa na fedha za barabara, maji na mengine. “Kwahiyo katika hizo fedha za MCC, zilizokuwa za Umeme hazivuki theluthi moja,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Muhongo, MCC ambao walitangaza kusitisha msaada wake kwa Tanzania ikiwa ni sehemu ya adhabu yake kwa kufanyika kwa uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar na utekelezaji wa sheria ya makosa ya mtandao, walikuwa wameamua kusaidia mradi ambao tayari Serikali ilikuwa imejitosheleza kwa kiasi chake kuufanya. Kwa mfano alioutoa, unaonesha MCC waliuongezea nguvu mradi huo lakini sio kuufadhili moja kwa moja.

SERIKALI YATAKIWA KUBOREESHA BAADHI YA MAPUNGUFU KWENYE MWENDOKASI
Maswahiba Wa Coastal Union Kufahamika J'pili