Kocha wa Klabu ya Pyramids FC ya Misri, Ehab Galal amesema amekiandaa vyema kikosi chake kuelekea mchezo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Azam FC.

Wababe hao wa Misri, tayari wameshawasili jijini Dar es salaam tangu Jumatano (Oktoba 13) na tangu jana Alkhamis (Oktoba 14) wamekua wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, kukamilisha maandalizi ya mchezo huo utakaoanza majira ya saa tisa alasiri kwa saa za Afrika Mashariki.

Kocha Ehab amesema kikosi chake kipo kamili kuelekea mchezo huo, lakini amejipanga kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya wenyeji wao (Azam FC), ambao watahitaji kupata matokea katika Uwanja wao wa nyumbani.

Amesema wamewafuatilia Azam FC kwa kuangalia baadhi ya Michezo yao, wamebaini wana ubora mkubwa wa kupambana wakati wote, hivyo itamlazimu kuwahimiza wachezaji wake kuwa na tahadhari ndani ya dakika 90 za mchezo wa kesho Jumamosi (Oktoba 16).

“Tumeangalia michezo yao kadhaa, ni timu nzuri iliyojipanga na imara zaidi kuliko timu zote zilizofuzu hatua hii ya kwanza kutoka kule kwenye mtoano,” amesema Ehab

“Lakini lengo letu ni kushinda mechi zote mbili na kusonga mbele, msimu huu tunalitaka hili Kombe.”

“Tunaelewa mazingira ya Dar es Salaam na tumejiandaa kupata matokeo chanya, kabla ya kurudi Cairo,” alisisitiza Kocha huyo mwenye presha kubwa ya kutakiwa kuipa Pyramids mafanikio.”

Mchezo huo wa Kombe la Shirikisho ‘CAF’ utakuwa wa pili kwa Azam FC, baada ya kuing’oa Horseed FC ya Somalia jumla ya mabao 4-1, huku Pyramids FC utakua mchezo wao wa kwanza msimu huu, kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la soka Barani Afrika ‘CAF’.

Mlipuko waua 7 Afghanistan wakati wa Ibada
Wachezaji 27 kwenda Botswana