Meneja wa muda wa klabu ya Real Madrid Santiago Solari amesema kikosi chake kinapaswa kuonyesha utofauti mkubwa katika mchezo wa kombe la Mfalme utakaowakutanisha dhidi ya Melilla, leo Jumatano.

Solari ameyasema hayo siku moja baada ya kutangazwa kuwa meneja wa muda wa kikosi hicho, kufuatia kufukuzwa kwa aliyekua mkuu wa benchi la ufundi klabuni hapo Julen Lopetegui, kutyokana na mabingwa hao wa barani Ulaya kuwa na mwenendo mbaya katika michezo ya ligi, kulikoambatana na kufungwa mabao matano kwa moja dhidi ya FC Barcelona mwishoni mwa juma lililopita.

Solari kwa mara ya kwanza aliongoza mazoezi ya kikosi cha Real Madrid kuanzia jana Jumanne, na alitumia muda wa dakika kadhaa kuzungumza na wachezaji na kuwaeleza nini wanachotakia kukifanya katika maandalizi ya kuelekea mchezo wa leo.

Baada ya kufanya kikao na wachezaji, Solari alizungumza na waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa: “Nimezungumza na wachezaji mambo mengi, jambo kubwa nimewahusia suala la kupambana na kusahau yaliyopita, soka halina tabia ya kukumbuka kilichotokea jana ama juzi, tumefungua ukurasa mpya ili tupate matokeo mazuri katika kipindi changu cha mpito.

“Wachezaji wamenionyesha kuwa tayari kupambana, wamenihakikishia hawatowaangusha mashabiki wa Real Madrid kuanzia mchezo wa kesho (Leo), ninaamini hakuna kitakachoshindikana, zaidi ya kupata ushindi.”

“Ninashukuru nimekabidhiwa timu yenye wachezaji wanaojua thamani ya ubingwa, nimetumia mwanya huo kuwaeleza namna ya kuendelea kuheshimika kama mabingwa, kwa kupambana uwanjani wakati wote, tena bila kukata tamaa.”

Solari mwenye umri wa miaka 42, anatarajiwa kuwa meneja wa muda wa kikosi cha Real Madrid kwa muda wa majuma mawili, na kisha uongozi wa Real Madrid utamtangaza meneja mpya wa kikosi hicho.

Futeni picha za ngono kwenye simu zenu- Makonda
Majaliwa atoa agizo kuhusu eneo la Kata ya Kiomoni