Kiungo kutoka nchini Hispania Santi Cazorla amesema bado anapenda kuendelea kubaki na klabu yake ya Arsenal ya Uingereza, licha ya baadhi ya vyombo vya habari vya nchini kwao kuanzisha tetesi za kutakiwa na Atletico Madrid.

Cazorla mwenye umri wa miaka 31, ametangaza msimamo wa kutaka kuendelea kubaki Emirates Stadium, huku mkataba wake ukitarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.

Cazorla amesema yupo tayari kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo inayonolewa na Arsene Wenger ambaye alimsajili mwaka 2012 akitokea Malaga CF.

“Nimekua na maisha ya furaha tangu niliposajiliwa na Arsenal. Ninaaminiwa na meneja pamoja na wachezaji wenzangu. Ninajiona ni mtu mwenye umuhimu mkubwa sana hapa, na kama nitapewa mkataba mpya nitakuwa mwenye furaha zaidi,” Amesema Cazorla alipohojiwa na kituo cha redio cha nchini Hispania kiitwacho Cadena Ser.

Kwa msimu huu wa 2016/17, Cazorla ameshafunga mabao mawili na anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachoanza katika mchezo ujao wa ligi kuu ya Uingereza dhidi ya Swansea City utakaochezwa Oktoba 15.

Joey Barton Haishiwi Vituko
Simba SC Waitaka Radhi Serikali Ya John Pombe Magufuli