Serikali imesema haitasita kuwaondoa katika nyadhifa zao Wakurugenzi wote watakaoshiriki katika kutoa taarifa za uongo kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Morogoro mara baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, ambapo ameeleza pia kuwa Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo  kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakiandika taarifa za uongo kuwa mradi umekamilika wakati haujajengwa, hivyo wakurugenzi watakaoshiriki kutoa taarifa zisizokuwa sahihi wataondolewa.

Alisema alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakurugenzi katika halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatembelea miradi yote inayojengwa katika maeneo yao ili kufanya ukaguzi na kujiridhisha kama thamani yake inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa.

Aidha Waziri Mkuu amesema Serikali aihitaji Halmashauri kutoa ajira za mikataba kwenye kada zilizopo katika muundo wa ajira hivyo ameziagiza halmashauri zote nchini kufanya mapitio ya watumishi wa mikataba.

“Tumeruhusu kuajiri kwa mikataba walimu wa masomo ya sayansi kwa kipindi cha miaka miwili tena kwa waliostaafu. Kuna kada zilizoko katika muundo wa ajira hizo hatuhitaji watumishi wa mikataba wakiwemo madereva msiwatumikishe kwa mikataba watakosa stahili zao,” alisema.

Majaliwa amezungumzia pia suala la watumishi hewa mkoani Morogoro amesema ni vema wakaendelea kufanya uchunguzi na ifikapo mwisho wa mwezi huu wawe wamekamilisha taarifa na kuanza kuchukua hatua kwa waliohusika kwa waliohusika.

Akiwasilisha taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Stephen Kebwe amesema mkoa unaendelea kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuzitaka taasisi zote za Serikali kufanya uhakiki wa mishahara hewa na malipo batili ya watumishi.

Kebwe amesema mkoa umebaini watumishi hewa 315 ambao wameisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 2.132 ambapo timu ya uhakiki bado inaendelea na zoezi hilo na taarifa kamili itatolewa mara kazi hiyo itakapo kamilika.

Lowassa afunguka kuhusu 'kuimbiwa' na kusemwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM
Majaribu: Chadema watangaza maandamano hadi 'Chato'