Upambanaji wa Kikosi cha Mbeya City msimu huu 2022/23 umemshutua Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddin Nabi na kuvuruga mpango wote wa kikosi chake kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbeya City imekua ikizungumzwa sana baada ya kuwakomalia Simba SC juzi Jumatano (Novemba 23), na kulazimisha sare ya 1-1, ikiwa nyumbani Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Kocha Nabi amesema amelazimika kuwazuia wachezaji wake kurejea katika familia zao baada ya kutua jijini Dar es salaam wakitokea mkoani Singida, na badala yake wameanza mapema kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Mbeya City.

Amesema katika kuzingatia hilo, wametumia muda wa kuutazama kwa pamoja mchezo wote waliocheza dhidi ya Simba SC na kubaini mazuri na udhaifu wao wanapokua Uwanjani, hivyo anaamini hatua hiyo itawasaidia kupambana vizuri kesho Jumamosi (Novemba 26).

“Nimekuwa na utamaduni wa kutoa mapumziko kwa wachezaji wangu mara baada ya mchezo kwa kuwaruhusu kurejea majumbani kwao kwenda kuangalia familia.”

“Lakini safari hii nimesitisha utaratibu huo kwa kuwataka wachezaji wote kuingia kambini mara baada ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC tulioucheza mkoani Singida.”

“Wachezaji na Benchi la ufundi tumeuona mchezo huo kwa dakika zote 90 na kuhimizana kuwa tuna kibarua kigumu katika mchezo huo kutokana na ubora wa wapinzani wetu.” amesema Kocha Nabi.

Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 29 sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya pili, huku Simba SC ikiwa nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 28.

Mbeya City ambayo itakutana na Young Africans Uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam Kesho Jumamosi (Novemba 26), ipo nafasi ya Sita ikiwa na alama 19.

Aziz Ki aongeza mzuka Young Africans
Ujio mpya wa Marioo na 'The Kid You know'