Mabingwa wa soka Tanzania bara Young Africans, wameshindwa kuutumia vyema uwanja wa Taifa kwa kukubali kupoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano wa ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Township Rollers kutoka nchini Botswana.

Young Africans waliokua nyumbani, wamejikuta wakikubali kufungwa mabao mawili kwa moja, ambayo yanawaweka njia panda katika harakati zao za kutinga kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza, Township Rollers ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 11 kupitia kwa Lemponye, lakini Young African walifanikiwa kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji wao kutoka nchini Zambia Obrey Chirwa dakika ya 30.

Katika kipindi cha pili kila timu ilionyesha umahiri wa kupambana huku zikishambuliana kwa zamu, lakini milango yote ilikua migumu hadi dakika ya 83, ambapo wageni Township Rollers walifanikiwa kupata bao la pili na la ushindi lililofungwa na Mosolesi Sikele.

Matokeo hayo yanaipa wakati mgumu Young Africans kuelekea mchezo wa mkondo wa pili ambao utachezwa mjini Gaborone nchini Botswana baadae mwezi huu.

Endapo Young Africans itahitaji kusonga mbele na kutinga kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika, italazimia kusaka ushindi wa mabao mawili kwa sifuri ugenini.

Mashabiki wa Arsenal waanzisha vuguvugu la kumng'oa Wenger
John Bocco: Historia inatubeba kwa waarabu