Kamati ya utendaji ya klabu ya Stand Utd, imeshindwa kufikia hatua ya kuvunja mkataba wa kocha Patrick Liewig kwa kigezo cha kuandamwa na matokeo mabaovu katika michezo minne mfululizo ya ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Kamati ya utendaji ya klabu hiyo, ilikutana kupitia taarifa iliyowasilishwa kwao na kamati ya ufundi ambayo ipo juu ya kocha huyo kutoka nchini Ufaransa, huku suala kubwa likiwa ni kushindwa kufanya vyema kama ilivyokua mwanzoni mwa msimu huu katika michezo ya ligi.

Kamati ya ufundi ambayo inaongozwa na Muhibu Kanu, inaamini kufanya vibaya kwa timu ya Stand Utd kunatokana na kocha Liewig, kushindwa kuwatumia baadhi ya wachezaji wenye uzoefu huku kigezo anachokitumia ni utobu wa nidhamu.

Liewig, anatuhumiwa kuwa na maelewano mabaya na baadhi ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza kama Harouna Chanongo, Rajab Dhahiri, Abuu Ubwa, Amry Kiemba pamoja na Eliasi Maguri anayeongoza kwa upachikaji wa mabao klabuni hapo.

Kanu amesema Kocha Liewig amekuwa hawatumii wachezaji hao muhimu huku akijua kuwa kikosi chake kinahitaji matokeo mazuri ili kijihakikishie kubaki kwenye ligi msimu ujao lakini amekuwa akipuuza hilo,na kama akiamua kumtumia mchezaji mmoja kati ya hao basi humpa dakika kumi au kumi na tano na baadaye anamtoa uwanjani huku akimsindikiza kwa maneno makali.

“Kwakweli huyu kocha sijui nini anaitakia timu yetu? kwa sababu anajua kabisa kwamba hao ni wachezaji muhimu kwenye klabu yetu na matokeo mabaya tunayoyapata kwa wakati huu ni kutokana na kuwaweka kando”

Kikao hicho cha kamati ya utendaji kimekubaliana kwa kauli moja kwamba kocha huyo ataendelea na kibarua chake mpaka msimu utakapomalizika kwakuwa hata mkataba wake pia unamalizika baada ya msimu huu kwisha.

“Kikao kimefanyika cha kamati ya utendaji lakini tumeona hakuna haja ya kumuondoa kocha kwa wakati huu wakati tumebakiza mechi tisa tu ili kumaliza ligi”

Kuhusu kipengele ambacho kipo kwenye mkataba wa klabu na kocha cha kwamba akipoteza mechi nne mfululizo mkataba utakuwa umevunjika, Kanu amesema wameamua kufunika kombe mwanaharamu apite na kukisamehe kipengele hicho kwa kumuacha amalizie kibarua chake.

Ruud Gullit: Nipo Tayari Kubebeshwa Gunia La Misumari
Valencia Wamtumia Ujumbe Mzito Jose Mourinho