Katika kuadhimisha wiki ya mlipa kodi, Wafanyakazi wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Katavi wamefanya usafi Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Katavi na kutoa msaada kwa mama wa mtoto mwenye changamoto ya tumbo kujaa maji.

Msaada huo ulitolewa baada ya kufika kwenye wodi ya watoto na kukutana na mama wa mtoto huyo ambaye amelazwa Hospitalini hapo na kumchangia zaidi ya shilingi laki mbili ili imsaidie katika mahitaji mbalimbali ikiwemo vipimo na dawa.

Mhudumu wa Afya (mwenye kilemba cheusi), akiwa na sehemu ya Watumishi wa TRA Mkoa wa Katavi ambao walifanya usafi Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Katavi na kutoa msaada kwa mama wa mtoto mwenye changamoto ya tumbo kujaa maji.

Mama wa mtoto huyo, Elizabeth Januari amesema, “Nimekaa naye kwa muda na hali ikawa inazidi kuwa mbaya nikamleta hapa Hospitali nikiwa sina chochote cha kumtibia huyu mtoto, nawashukuru TRA, Mungu awabariki sana.”

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Idara ya Watoto, Hospitali ya rufaa Mkoa wa Katavi, Dkt. Maria Matei amesema baada ya kumpokea Mama huyo walimuanzishia matibabu mtoto wake licha ya kwamba hakuwa na fedha, lengo likiwa ni kuimarisha afya ya mtoto kwanza.

Watumishi wa TRA wakijadiliana jambo na mtumishi wa Afya katika Hospitali hiyo.

Kwa upande wake meneja wa TRA Mkoa wa Katavi, Jacob Mtemang’ombe amesema baada ya kupokea taarifa za Mama huyo wakati wakiwa kwenye wodi ya watoto, waliguswa na kuchangishana ili kumwezesha mama huyo na kutoa wito kwa taasisi zingine kuwa na utaratibuwa wa kurudisha kwa jamii.

Waipinga Serikali uondoaji sheria ya uchochezi
UNHCR yawapa tabasamu Mahabusu na Wafungwa Katavi