Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Selemani Jafo ameahidi kushughulikia changamoto ya msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani VAT kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo katika utekelezaji wa miradi mingi ya serikali.

Ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa miradi ya soko na stendi mpya ya mabasi mkoani Njombe mara baada ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo iliyopo mjini Njombe.

“Kama mnakumbuka vizuri mwaka juzi tulikuwa tunazindua stendi ya Korogwe na wakati tunaongea nilimueleza Rais changamoto kubwa ni VAT, Rais alituagiza mimi, mwanasheria mkuu wa serikali, alimuagiza waziri wa fedha kwenda bungeni kufanya mabadiliko ya sheria na aliamua mpaka sheria ile iingie bungeni kwa hati ya dharula, sheria ile ikaingizwa bungeni kwa lengo kwamba miradi yote kama hii isiwe inatozwa VAT nadhani mnakumbuka,”amesema Jafo

Awali msimamizi wa miradi hiyo mhandisi, Tembo David amesema kuwa changamoto kubwa kwasasa inayowakabili wakandarasi ni msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani VAT kwa kuwa mpaka sasa wakandarasi hawajapata.

Aidha, waziri Jafo ameitaka Halmashauri ya mji wa Njombe kupata suluhu ya jambo lililokwamisha uwepo wa ujenzi wa kituo cha mafuta ndani ya stendi kama ilivyokuwa kwenye mchoro wa awali hatua ambayo inaifanya halmashauri hiyo pia kukosa mapato ili hali stendi hiyo ina eneo la kutosha.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri amemuahidi waziri Jafo kuendelea kusimamia kwa ushirikiano shughuli zilizosalia za ujenzi na kumwambia kuwa pale patakapohitaji msaada hawatasita kuwasiliana kwa ajili ya kuhakikisha kuwa changamoto zinatatuliwa ili Wananchi wa Njombe waweze kunufaika.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 2, 2019
Wanafunzi kutoka nchini Ireland wapanda Miti mkoani Njombe