Huko Simba SC mambo yameanza baada ya kocha Abdelhack Benchikha kumuachia msala kocha msaidizi, Selemani Matola kukiongoza kikosi hicho katika mazoezi ya timu hiyo hadi pale atakaporudi kuendelea na programu za maandalizi ya michuano ijayo.

Wachezaji wa Simba SC walipewa mapumziko ya siku 10 hadi jana jioni waliporejea kambini kuendelea na mazoezi huku kocha mkuu, Benchikha akitarajiwa kuwasili nchini muda wowote kuanzia leo baada ya kwenda kwao Algeria kwenye mapumziko.

Simba SC ilipewa mapumziko hayo ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mlandege katika fainali ya Kombe la Mapinduzi iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, Januari l3.

Mmoja wa kiongozi wa timu hiyo ambaye hakutaka jina lake kutangazwa hadharani amesema, kwa sasa Matola atasimamia mazoezi ya kikosi hicho kwa kufuata programu zote za kocha mkuu alizomtumia hadi atakapowasili muda wowote kuanzia leo.

“Mazoezi atakayoanza nayo taratibu ni kukimbia kwanza kwa hizi siku chache, kuchezea mpira, lengo ni kuweka miili sawa baada ya baadhi yao kutokuwa na michezo ya kiushindani kwa wiki hizo mbili kisha watahamia Gym na kwingineko,” amesema kiongozi huyo.

Kiongozi huyo ameongeza licha tu ya Matola kupewa nafasi hiyo ila atasimamia pia timu ya vijana ya Simba SC kwani kocha wa kikosi hicho, Mohamed Mulishona ‘Xavi’ anayeifundisha amepewa jukumu la kuisimamia timu ya taifa ya Wanawake ya chini ya miaka 17.

Alipotafutwa Matola ili kufahamu kuhusu programu hiyo ambapo alikiri timu hiyo inaanza mazoezi lakini hakuingia kwa undani.

“Kocha mkuu ndiye anatakiwa kuzungumza kuhusu mazoezi, lakini ninachofahamu ni kwamba tumeanza tangu jana, mengine tutaendelea leo,” amesema Matola mchezaji wa zamani wa Simba SC.

Simba SC inaingia kambini ikiwa na mzuka mpya baada ya maingizo ya wachezaji sita wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 16, mwaka huu ili kuongeza nguvu kufuatia kutokuwa na msimu mzuri tofauti na mahasimu wao Young Africans.

Nyota wapya ni Edwin Balua, Saleh Karabaka, Ladaki Chasambi, Fredy Michael Kouablan, Babacar Sarr na Pa Omar Jobe.

Watakiwa kutowatelekeza Watoto kisa huduma
Vitisho sababu Chamisa kujiuzulu CCC