Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi – CCM, Mkoa wa Pwani, Mwinyishehe Mlao amewataka wanaCCM kujenga umoja na msikamano wakati huu ambapo wanaelekea kwenye chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji na uchaguzi Mkuu wa mwakani, ili CCM ipate ushindi wa kishindo na kuendelea kubaki madarakani.

Amesema hayo wakati wa kilele Cha sherehe za maadhimisho ya Miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM Mkoa wa Pwani katika Kijiji cha Fukayosi kilichopo Wilaya ya Bagamoyo, ambapo wanaCCM walikusanyika kushiriki shughuli mbalimbali za utekelezaji wa ilani.

Amesema, wakati wa uchaguzi kila mpiga kura ahakikishe anawachagua Viongozi wa Serikali wenye nia njema ya kuongoza na si kwa ajili ya maslahi yao binafsi kwani kufanya hivyo ni kupoteza haki za wengine.

“Tusikubali kusababisha migogoro isiyo na tija tunapoelekea kwenye chaguzi zijazo na wala tusikubali watu watugawe kwa ajili ya maslahi yao,” alisema Mlao.

Awali akimkaribisha Mwenyekiti huyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani, Bernard Ghati alisema sherehe za maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM Mkoani Pwani zilianza tangu Januari 28, 2024  ambapo uzinduzi ulifanyika katika Kata ya Mlanzi, Wilayani Kibiti.

Mbali na utekelezaji wa shughuli mbalimbali, pia Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Pwani alikabidhi sare za Shule, Madaftari na Kalamu kwa Wanafunzi walio katika mazingira magumu na Watoto yatima wa Shule za Msingi na Sekondari.

Watumishi wa Umma acheni dharau - Lusinde
Wahimizwa kutunza hifadhi Mlima Hanang'