Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kuwa Mradi Mkubwa wa Uchimbaji Madini Tembo unaotarajiwa kutekelezwa Wilayani Pangani Mkoa wa Tanga utaiweka Tanzania katika ramani ya dunia.

Mavunde ameyasema hayo alipotembelea eneo la Tajiri lililopo wilayani humo ambako Mradi huo unaotarajiwa kutekelezwa na Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited yenye ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Strandline Resources Limited kutoka nchini Australia mara baada ya utaratibu wa upatikanaji leseni kukamilika.

Amesema, Mradi huo utasaidia kutangaza fursa zilizopo nchini za madini hayo duniani pamoja kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi nchini pamoja na pato la mtu mmoja mmoja kwa kutoa nafasi za ajira kwa wananchi na wenyeji wa Pangani.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Madini, leseni kubwa ya uchimbaji wa madini [Special Mining License – SML] inatolewa na Baraza la Mawaziri kwahiyo tunasubiri vikao vya Baraza la Mawaziri kwakuwa tumeshakamilisha taratibu kwa kushirikisha taasisi mbalimbali zinazohusika pamoja na wananchi wenyeji wa Pangani ambao wameonyesha kuwa wameukubali na wanautaka mradi” amesema Mavunde.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya Pangani, Zainab Abdallah amesema kuwa Mradi huo wa kwanza kuwa na leseni kubwa ya uchimbaji wa madini mkoani Tanga utasaidia kufungua fursa za ajira kwa wakazi wa wilaya hiyo kupitia ushirikishwaji wa Watanzania katika mradi (Local Content) pamoja na wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) huku akikaribisha wawekezaji wengine kwenda kuwekeza katika wilaya hiyo.

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited kwa upande wa Serikali, Mhandisi Heri Gombera amesema kuwa Mradi huo unatarajiwa Tani milioni 8 kwa mwaka ya Madini Tembo na kutokana na utafiti wa sasa unaonyesha kuwa uhai wa mgodi huo ni kati ya miaka 20 hadi 25 ambapo katika kipindi hicho makusanyo ya Serikali yanakadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 457.24 sawa na shilingi trilioni 1.145.

Madini hayo hutumika katika mitambo ya nyuklia pamoja na kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo mapambo, vifaa tiba, injini za ndege, saa, simu, kompyuta mpakato (laptop) na vyungu vya kuyeyushia metali pamoja na kutengenezea marumaru.

Utata waibuka kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Mawaziri DRC
Tanzania yashiriki Mkutano ubunifu teknolojia za Maji