Wakati watu watu wengi wakimmwagia sifa kiungo wa Young Africans, Stephene Aziz Ki kwa kazi kubwa anayofanya uwanjani, nyota huyo amesema mtaalumu zaidi ni Mudathir Yahya.

Aziz ambaye amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu akiongoza kwa kupachika mabao Ligi kuu Bara baada ya kufunga 10, Jumamosi (Februari 24) alikimbia na kwenda kumfuta kiatu Mudathir alipofunga bao la kwanza dhidi ya CR Belouazdad, amesema staa huyo ana mguu wa dhahabu.

“Mudathir alivyofunga bao la kwanza nilienda kubusu kiatu chake. Yule jamaa ana mguu wa dhahabu kwani tulitumia zaidi ya dakika 40 kutafuta bao bila mafanikio hadi alipofunga kitaalamu. Ni mchezaji hatari zaidi kikosini, anaweza kucheza maeneo karibu yote.

“Kuna muda alicheza kama namba sita wakati mwingine namba nane na hata namba 10 na huko kote anacheza kwa ubora wa hali ya juu. Huo ndio utofauti wake na wengine kwani anafanya vitu vingi ambavyo kila kocha atapenda,” amesema Aziz Ki aliyefunga bao la pili kwenye ushindi mabao 4-0 ilioupata Yanga mbele ya Belouizdad, huku mabao mengine yakifugwa na Kennedy Musonda na Joseph Guede.

Staa huyo amesema pamoja na Mudathir kuwa bora lakini pia ubora na maelewano ya kikosi kizima cha Young Africans ndio nguzo ya mafanikio kwa timu hiyo.

“Kila mchezaji anacheza kwa kumtegemea mwingine. Young Africans ina kikosi bora hivyo hiyo ni faida kwa kila mmoja wetu. Hauwezi kuwa bora kama hauchezi na watu bora,” amesema.

Kiungo huyo aliyejiunga na Young Africans msimu uliopita katika kipindi cha dirisha dogo akiwa mchezaji huru baada ya kuachwa na Azam FC, amekuwa na mchango mkubwa kikosini hapo.

Mchezaji huyo tegemeo wa timu ya taifa “Taifa Stars’ hadi sasa ameifungia Young Africans mabao sita na asisti mbili kwenye ligi na moja katika Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akisifika maeneo mengi uwanjani.

Akizungumza jijini Dar es salaam Mudathir amesema siri ya ubora wake ni kufuata maelekezo na kujituma: “Siri kubwa ni kujituma na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi.

“Ukiangalia eneo la kiungo kwa Young Africans limeshteheni mastaa kibao wenye uwezo hivyo ni chachu kwangu kupambana zaidi na kuonyesha ubora.”

Maandamano ya siri yamuibua Diwani Bahi
Benchikha achora ramani ya maangamizi