Mkaguzi Kata ya Kiutu Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha, Tunu Makwaya Pingu amewaasa vijana wa kata hiyo kujikita katika shughuli za maendeleo huku akiwata kutojihusisha na dawa za kulevya ambazo zimekuwa zikipoteza nguvu kazi ya vijana.
Mkaguzi Tunu ameyasema hayo wakati alipowatembelea Vijana wanajihusisha na shughuli za ufyatuaji wa matofali ambapo amewapongeza kwa kujituma katika kazi ambayo itawaongezea kipato wao pamoja na familia zao.
Amewaomba Vijana hao, kuwa mabalozi wazuri kwa vijana wengine wa kata hiyo ambayo hapo awali vijana wengi wa eneo hilo walionekana kujihusisha na dawa za kulevya huku akiwapongeza vijana hao ambao kwa sasa wameachana na vitendo hivyo.
Aidha, Tunu pia amewaomba vijana hao kuwa namba moja katika kufichua uhalifu katika kata hiyo ambayo kijografia inapata wageni wengi wa mataifa ya afrika na ulaya katika shughuli za utalii.
Hata hivyo, amewaambia kuwa usalama ukiwa wa kutosha katika kata hiyo wategemee kukua kiuchumi kwani watu wengi watapenda kufika katika kata hiyo.