Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi – CCM, Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali chini ya utawala wa CCM imedhamiria kufanya uchaguzi huru na wa haki kuanzia wa Serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025.
Kinana ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu akimwakilisha Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mkutano mkuu wa chama cha ACT -Wazalendo.
Amesema, “tunakwenda katika uchaguzi wa serikali za mitaa na baadaye mwakani uchaguzi mkuu. Kumefanyika mabadiliko ya sheria tatu bungeni. Sheria ya vyama vya siasa, sheria ya tume ya uchaguzi na sheria ya uchaguzi.”
“Nataka niwahakikishie kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ina dhamira ya dhati katika mwaka huu wa uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka ujao kwenye serikali kuu kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki,” amesema Kinana.
Aidha ameongeza kuwa, mbali na kupitisha sheria nzuri ya kuhakikisha kunakuwapo uchaguzi huru na wa haki, pia dhamira ya Rais Dkt.Samia kufanikisha hilo inajipambanua katika utekelezaji wake.

SJMT, SMZ watatua hoja 21 za Muungano
Ndejembi: Wanafunzi la saba, kidato cha kwanza wasajiliwe kwa wakati