Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeanza rasmi nchini ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhakikisha kuwa Wananchi na hasa kina mama wanahama kutoka matumizi ya nishati ya kupikia isiyo safi, kwenda kwenye nishati iliyo safi na salama.

Dkt. Biteko ameyasema hayo Wilayani Temeke Mkoani Dar es Salaam, wakati wa hafla ya ugawaji mitungi ya gesi na majiko banifu kwa wajasiriamali katika Soko la Temeke Stereo na Mbagala Zakhem.

Amesema, “nataka niwaeleze kuwa, safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeanza katika wiki hii ambayo tunasherehekea siku ya Wanawake Duniani kwa sababu tunafahamu kwamba Mwanamke ni mwathirika mkubwa nishati isiyo safi ya kupikia na wanapata madhara mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa kifua, kubakwa na kutumia muda mrefu kutafuta kuni hivyo Serikali imeona kuwa ina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi ili kumwezesha mwanamke kupata nishati safi na kwa gharama nafuu.”

Amesema, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia siyo tu kwa Tanzania bali Afrika nzima na ulimwenguni; na hii ilithibitika wakati akizindua Programu ya Nishati safi ya kupikia itakayosaidia Wanawake Barani Afrika (African Women Clean Cooking Support Programme (AWCCSP) katika Mkutano wa Cop 28 Dubai ambayo imeungwa mkono na wadau mbalimbali hivyo kama nchi lazima iwe na mpango maalum wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Aidha, ameongeza kuwa, zoezi hilo la ugawaji wa mitungi ya gesi na majiko banifu halitaishia Dar es Salaam bali ni endelevu na litafanyika katika mikoa mbalimbali nchini ili wananchi katika maeneo yote wahamasike kutumia nishati safi ya kupikia.

Ujumbe wa Mhandisi Mahundi kwa Wanawake wote
Kuelekea uchaguzi Mkuu: Urusi yaishukia Marekani