Heldina Mwingira.

Machi 8 tulishuhudia kilele cha siku ya Wanawake Duniani. Ndani ya siku hii vitu mbalimbali vilifanywa na Wanawake kama vile kukutana na kujadiliana kuhusu mafanikio, changamoto, namna ya kutatua changamoto hizo na mustakabali wa maisha yao.

Kwa mwaka huu 2024 kauli mbiu yao ilisema “Wekeza kwa Mwanamke, kuharakisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa Jamii.” kauli hii inaendelea kuthibitisha kuwa ukimuendeleza mwanamke umeendeleza jamii.

Tukiwa tunaunga mkono kauli mbiu hii  Dar24 Media inaangazia namna gani  Wanawake wachuuzi wa Samaki katika maeneo ya Tabata  ndani ya Jiji la Dar es salaam wanavyoweza kuendesha maisha yao kupitia biashara hiyo na changamoto wanaokumbana nazo.  Mmoja wa Wafanyabiashara hao ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Bi Swaumu alisema amepata mafanikio kupitia biashara ya samaki, inamsaidia  kwa kuwalipia ada  watoto wake na kuendesha maisha yao ya kila siku.

Alisema, mfumuko wa bei wa Samaki ni changamoto kubwa kwano na wakati mwingine husababisha kushindwa kununua Samaki na hata wakinunua  wanapata hasara, kwasababu wateja wao huwakimbia.

Anasema, Biashara hiyo pia imekuwa ni hatarishi kwa ndoa yake kwani mume wake hamuamini akihisi anamsaliti kutokana kuamka saa 10 alfajiri na kuchelewa kurudi.

“Natoka saa 10 kamili kwenda feri na nikifika kule kama nikikuta bei ni kubwa inanilazimu kusubiri mpaka samaki watakaovuliwa mchana na nikiona bei kubwa  bado inapelekea kusubiri samaki wa jioni,’  alifafania Bi. Swaumu.

Kwa upande wake Bi. Asha Athumani yeye alisema, ‘kutokana na gharama za maisha kupanda inapelekea wakati mwingine kula mtaji wote na kupata mtaji ni changamoto maana wanaume wetu hawatupatii mtaji hivyo inatulazimu  kukopa mikopo ya  kausha damu.”

Anasema, ‘mikopo ya kausha damu inauma kwasabababu tunafanya biashara kwa ajili ya marejesho na ikitokea umechelewa kulipa wanakufilisi na naishauri serikali iondoe mikopo ya namna hii haitusaidii inatuumiza.’

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani uliopo kata ya Liwiti huko Tabata Dar es Salaam, Grace Bruno alizungumzia kuhusu mikopo umiza kwa Wafanyabiashara wakiwemo Akina mama wauza Samaki.

Alisema, ‘katika migogoro ya wananchi na  taasisi za mikopo inayojulikana kama kausha damu, najitahidi sana kuishughulikia kwa kuzungumza kwa kutumia busara kwa viongozi wa taasisi hizo na nimefanikiwa kuwasaidia wananchi wa mtaa wangu kutofilisiwa’

Hata hivyo, akatoa rai kwa taasisi za kifedha kuwa, ‘Kabla ya kukopesha inapaswa  watoe elimu kwa Wananchi  na kusisitiza  taasisi za kifedha ziwe ni kwa ajili ya  kuwainua wanawake na sio kuwakandamiza.’

Kwa kuondoa au kupunguza vikwazo kwa wanawake katika biashara zao au sekta yoyote wanayoitumia kujikwamua kutasaidia kuwa sehemu ya uwekezaji kwa wanawake na hivyo maendeleo yatapatikana mapema na kwa wepesi.

Hata hivyo, kiujumla ulimwenguni bado unakabiliwa na migogoro ya umasikini, ukosefu wa usawa na sehemu kubwa inawakumba Wanawake ikiwemo ya unyanyasaji wa kazi na unyanyasaji wa kijinsia wa watoto katika majukwaa ya burudani.

Kwa kuwekeza kwa wanawake, tunaweza kuibua mabadiliko na kuharakisha mpito kuelekea dunia yenye afya, usalama na usawa zaidi kwa wote na ikumbukwe kwamba, UN inaonya kuwa migogoro na kupanda kwa bei kunaweza kusababisha 75% ya nchi kupunguza matumizi ya umma ifikapo 2025, na kuathiri vibaya wanawake na huduma zao muhimu.

Ni wazi kuwa siku hii imetoa fursa ya kuashiria maendeleo yaliyopatikana, lakini pia kuangazia mmomonyoko wa haki za wanawake duniani kote, pamoja na madhara ya unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji.

Kwa mujibu wa kielezo cha Global la Jinsia Duniani cha mwaka 2023, kinachochapishwa kila mwaka na Jukwaa la Kiuchumi la Dunia, kinabainisha kuwa hakuna nchi ambayo bado imefikia usawa kamili wa kijinsia au usawa.

Hivyo ni muhimu kuweka bidii kuhakikisha Wanawake wanapewa nguvu na ushirikiano katika kuyafikia malengo yao waliyojiwekea kupitia umoja wao na maazimio yaliyofikiwa Ulimwenguni.

 

 

 

Imani Kajula: Haitakuwa rahisi, lakini inawezekana
Hersi Said: Mamelodi Sundown ndio mpinzani halisi