Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Wakuu wa Mikoa kutenda haki kwa wananchi katika sekta ya ardhi na kuwasimamia Madiwani waache kumega vipande vya ardhi kwa maslahi yao binafsi.

Rais Samia amesema, baadhi ya migogoro ya ardhi inasababishwa na tabia ya viongozi wa Halmashauri kuongeza na kusajili vijiji vipya kwa njia za magendo kwa manufaa ya Madiwani ambao nia yao ni kujiongezea maeneo ya wapiga kura.

Rais Samia amesema hayo wakati wa hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa ya Songwe, Mtwara, Tabora, Shinyanga na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), iliyofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Ikulu.

Aidha, Rais Samia amewataka viongozi hao kusimamia na kutatua kero za wananchi zinazojitokeza katika maeneo yao kwa kuwa serikali inatoa fedha kupitia TAMISEMI, ili kutatua changamoto hizo.

Amewataka Viongozi hao kusimamia mifumo ya ukusanyaji mapato, ili kupandisha makusanyo ya Halmashauri bila kuleta usumbufu kwa wananchi pamoja na kuzuia mitandao inayochepusha fedha zinazokusanywa.

Hata hivyo, Rais Samia pia amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa kuzingatia katiba, sheria na taratibu za utumishi wa umma na kuacha kuvunja mikataba na wakandarasi bila kufuata miongozo ya kisheria kwa mujibu wa mikataba.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Wakuu wa Mikoa kuhamasisha shughuli za maendeleo na kusaidia wananchi kupata elimu ya fedha (financial literacy), ili shughuli wanazozifanya zibadili maisha yao.

ASDP II kuleta mapinduzi sekta ya Kilimo
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 14, 2024