Sekta ya elimu imetajwa kuwa ni wakala wa mabadiliko katika jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni katika kuleta maendeleo ya nchi na kwamba utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya vipaumbele vya nchi katika kuleta maendeleo.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa mkutano wa wadau wa Sekta ya Elimu mkoani Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Biblia-TAG jijini Dodoma.

Amesema “ili kufanikisha haya tunahitaji sekta hii kuwa bora, imara, inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa.”

Majaliwa ameongeza kuwa, Rais Dkt. Suluhu Samia ni mdau namba moja wa sekta ya elimu na ndio maana katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake amewekeza katika kuweka mazingira bora ya utoaji elimu na kuhakikisha Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo katika Sekta ya Elimu.

“Sisi sote ni mashuhuda wa jinsi Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan alivyotekeleza kwa vitendo azma ya kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa Watoto wote wa Kitanzania. baadhi ya maeneo ambayo ameyasimamia ni Mpango wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu, Ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi, Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Mapitio ya Sera Ya Elimu na Mafunzo,” amesema.

Ameyataja maeneo mengine kuwa ni Kuimarisha Usimamizi wa Sekta ya Elimu kwa kutoa vyombo vya usafiri kwa viongozi wasimamizi wa elimu pamoja na wathibiti ubora wa shule, Kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji Elimu na kutoa Mafunzo kwa walimu kazini (MEWAKA) kwa ajili ya kuwajengea uwezo na umahiri katika kutimiza majukumu yao.

Themba Zwane kuikosa mechi ya Dar
Wahimizwa matumizi sahihi Miundombinu Majitaka