Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma – DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amewataka Wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya utumiaji wa mfumo wa mtandao wa majitaka, ili kuondokana na adha ya kuziba mara kwa mara kwa mitandao hiyo.

Aron ameyasema hayo hii leo Machi 26, 2024 wakati alipotembelea Kata ya Majengo, Mtaa wa Kitenge eneo lililoathiriwa na kujaa kwa Majitaka kwa lengo la kukagua na kujionea hali ya mazingira katika eneo hilo na kudai kuwa uzibaji wa mara kwa mara katika mifumo ya majitaka sio kwa sababu ya majitaka kuwa mengi, bali ni kuingizwa kwa vitu na taka ngumu ambavyo vinasababisha mfumo huo kuziba.

Amesema, “Maendeleo yanaenda na mambo mengi na yanagharama kidogo, na gharama yenyewe ndio kama hii, lakini isingekuwa hivi, kama wananchi wanazingatia matumizi sahihi ya mtandao wa majitaka. Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi watumie kwa sahihi mfumo wa majitaka, mfumo wa majitaka ni kwa ajili ya kutumia majitaka tu hata maji ya mvua hayatakiwi kuingia kwenye mfumo huo”

Akiongea katika eneo hilo, Diwani wa Kata ya Majengo, Shufaa Ibrahim ameishukuru DUWASA kwa kupokea malalamiko na kufika eneo lenye changamoto ili kujionea hali halisi na kuweza kutatua changamoto hiyo na kuahidi kuitisha mkutano wa wakazi wa eneo hilo na kuwaita wataalamu kutoka DUWASA ili waweze kutoa Elimu ya kutosha kwa wananachi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi Wa Mazingira DUWASA, Mhandisi Bernard Rugayi amesema kwasasa wanaendelea na zoezi la unyonyaji wa majitaka katika eneo hilo na ameahidi kumaliza changamoto hiyo kwa muda wa siku tano.

Majaliwa: Sekta ya elimu wakala mabadiliko kiuchumi
Ibrahim Imoro anasakwa Msimbazi