Gwiji wa Klabu ya Simba Abdallah ‘King Kibadeni’, ameliomba Benchi la Ufundi la timu yake hiyo kumpanga Mlinda Lango Ayoub Lakred katika mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Simba SC itaikaribisha Al Ahly katika Uwanja wa Benjamin Mkapa keshokutwa Ijumaa (Machi 29) kabla ya kwenda kurudiana Aprili 06, kwenye Uwanja wa Cairo, Misri na mshindi wa jumla atatinga Nusu Fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya vilabu Barani Afrika.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Kibadeni amesema ameangalia baadhi ya mechi ambazo makipa wote walicheza na kuona Manula ameshuka kiwango kidogo kutokana na majeraha ambayo aliyapata huko nyuma, huku Ayoub raia wa Morocco akiwa kwenye kiwango cha juu kwa sasa.

Amesema, licha ya Manula kupona na kurejea Uwanjani, lakini anaamini hajawa fiti jambo ambalo lilimfanya kuruhusu mabao matano katika mechi dhidi ya Young Africans.

“Tutampa lawama sana Manula, hivi karibuni hayupo katika ubora alikuwa nao awali, kwa sababu ametoka katika majeraha makubwa na anatakiwa kupewa mechi zisizo na ushindani mkubwa kwa sasa yule kipa kutoka Morocco (Ayoub) yupo vizuri apewe nafasi ya kucheza ikiwezekana hii mechi ya ljumaa (Machi 29) dhidi ya Al Ahly.”

Amesema anaimani kubwa kwa Simba SC kufanya vizuri dhidi ya Al Ahly.

“Sina mashaka na Benchi la Ufundi, wana kocha Benchikha (Abdelhak), mzuri ana uzoefu na hii michuano, kikubwa wachezaji wanatakiwa kuelewa kuwa wamebeba mioyo ya watu wengi,” amesema Kibadeni.

Ameongeza kuwa viongozi wanatakiwa kukaa na wachezaji nao kuhusu kuzungumza umuhimu wa mchezo huo dhidi ya Al Ahly, ili kupambana na kuwapa burudani mashabiki na wanachama ambao wanaumia pale Simba SC inapofanya vibaya.

“Binafsi nimekuwa na wakati mgumu sana juu ya Simba SC inapofanya vibaya, ninaimani katika mchezo wa keshokutwa Ijumaa (Machi 29) tutafanya vizuri, kikubwa Wanasimba tushirikiane na kuwa wamoja tukifanya hivyo tunaweza kumuondoa Al Ahly kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, alivyoondolewa Zamalek ya Misri,” amesema Kibadeni.

Kuhusu viwango vya wachezaji wawili, Freddy Michael na Pa Omar Jobe, waliosajiliwa dirisha dogo, amesema kama kocha hana mashaka na wachezaji hao na wanatakiwa kupewa muda.

“Ni mapema sana kuwazungumzia hao wachezaji hawana muda mrefu ndani ya timu, katika usajili hasa nyota wa kigeni kuna mambo mengi sana, kwanza ni mazingira ya kuyazoea, lakini na aina ya wenzake aliokutana nao katika timu husika, mfano ukimchukuwa Lionel Messi akija hapa atakuwa na ubora huo?,” amesema mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC anayeshikilia rekodi ya kufunga ‘Hat-Trick’ kwenye Dabi dhidi ya Young Africans.

Tanzania yamuahidi ushirikiano Rais mteule Senegal
Michael Olise aishughulisha Man Utd