Scolastica Msewa, Kibaha – Pwani.

Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge hii leo Machi 28, 2024 amesema atayafungia kupita mkoa wa Pwani mabasi yatakayoendelea kuvunja Sheria za Barabarani katika mkoa huo.

Kauli ya Kunenge inakuja baada ya watu wawili kufariki dunia na wengine watano kujeruhiwa wakiwemo Askari wa zimamoto kutokana na ajali ya magari matatu kugongana na Lori la mafuta kulipuka.

Amesema, “Na kama mtagundua mkoa wa Pwani hii Barabara ni kubwa na mabasi yakitoka kule standi kuu ya Dar es salaam Mbezi ni mabasi mengi yakiwa yamekaguliwa lakini bado hapa pia tunakagua pia” alisema RC Kunenge.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo amesema tarehe 28.03.2024 majira ya saa 10:15 alfajiri huko bonde la Ruvu, Wilaya ya Kipolisi Mlandizi, Mkoa wa Pwani barabara ya Morogoro Dar es salaam Gari namba T668 DTF aina ya Scania kampuni ya Sauli ikiendeshwa na dereva itwaye Idd Aloyce (35) lilipata ajali.

Amesema, Dereva huyo mkazi wa Mafinga alikuwa akitokea Dar es Salaam kuelekea Mbeya aliligonga ubavuni lori la mafuta ya Petroli lenye namba za usajiri RAF672N na tela lenya namba RL2594 aina ya Howo lililokuwa linatoka Dar kwenda Rwanda likiendeshwa na dereva aitwaye Mushimana Musiyimana lililokuwa limesimama kupisha gari lililokuwa linakuja mbele yake.

Aidha basi hilo lilikuwa limeongozana na basi la Golden Deer kampuni ya New Force lenye namba za Usajiri T175 DZU, likiendeshwa na Burton Jacob, miaka 33, mkazi wa Mbeya ambapo nalo lililigonga kwa nyuma basi la Saul lililokuwa mbele yake na kusababisha vifo vya watu wawili ambao hawakufahamika majina yao na majeruhi watatu amabo ni Salimu Daud, miaka 50, mkazi wa Mbozi, Farida Idrisa, miaka 26, mkazi wa Tabata Dar es salaam na Kiambile Geofrey, mkazi wa Uyole Mbeya.

Baada ya ajali hiyo, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zima moto na uokoaji wakiwa katika harati za kuwatoa marehemu waliokuwa wamenasia kwenye gari ghafla magari yaliwaka moto uliotokana na petroli iliyokuwa inavuja toka kwenye tenki la mafuta.

Jeshi la zimamoto na uokoaji lilifanikiwa kudhibiti moto huo na kuwatoa marehemu ambao nao walikuwa wameteketea kwa moto, kwa mara nyingine moto ulilipuka tena toka kwenye moja ya chumba cha tenki la mafuta na kusababisha majeraha kwa askari wawili wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji ambao ni Koplo Hamis Kungwi na Koplo Elias Bwire amabo walikimbizwa Hospitali ya Mloganzira kwa matibabu na hali zao zinzendelea vizuri.

Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa madereva wa mabasi yote mawili kushindwa kuchukua tahadhari kwa kuyapita magari mengine, lakini pia kushindwa kutunza umbali kati ya gari moja na lingine yakiwa yanafatana.

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya injini ya basi la Saul iliyokuwa imekita chini baada ya kugonga gari lingine na kulipua petroli wakati wa uokoaji.

Wito wa Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani ni kuwataka madereva kutii sheria za usalama barabarani kwa mujibu wa taaluma zao, kwani wanachukua dhamana kubwa ya maisha na mali za watu.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 29, 2024
CCM wabaini madudu miradi ya Afya, Barabara