Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, amekiri kuwa timu yake itakuwa na faida zaidi ya Manchester City katika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutokana na ratiba yao kuwa nyepesi.

‘Los Blancos’ hao watacheza na Man City katika hatua ya Robo Fainali, na mechi ya kwanza itafanyika Santiago Bernabeu Jumanne ya April 9, kabla ya mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Etihad Jumatano ya Aprili 17, mwaka huu.

Hata hivyo, kocha wa City, Pep Guardiola alifichua kuchoshwa kwake na mpangilio wa mechi wiki iliyopita huku timu yake ikiwa na ratiba ya Ligi Kuu England, wakati Madrid watakuwa na siku tisa za mapumziko.

“Tunacheza na Aston Villa saa 2:15, kisha saa 6:30 dhidi ya Crystal Palace Jumamosi,” alisema Guardiola.

“Kisha tunaenda Madrid Jumanne. Madrid ina siku tisa za kujiandaa.

“Wanacheza wikendi hii na hawatacheza tena hadi mchezo wetu. Ningependa kutafakari na kuomba siku moja zaidi, kwa sababu tofauti ni kubwa”

Kutokana na ushindi wa mabao 2-0 wa Madrid nyumbani dhidi ya Athletic Club Jumapili (Machi 31), Ancelotti aliulizwa maoni yake juu ya maoni ya Guardiola na akakubali kwamba timu yake itakuwa na faida.

“Naiona vizuri, wana ratiba ngumu zaidi. ni soka la kisasa.” alisema Ancelotti.

“Ni dhahiri kwamba tuna faida ndogo, lakini haitaathiri mechi.”

Madrid wamepangwa na City katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa kwa msimu wa tatu mfululizo baada ya kukutana nao katika Nusu Fainali katika kila moja ya kampeni mbili zilizopita.

Mshindi wa mechi hii atakutana na Mshindi wa mchezo wa Arsenal na Bayern Munich katika Nusu Fainali, huku Atletico Madrid, Borussia Dortmund. Paris Saint-Germain na Barcelona zikicheza upande mwingine wa droo.

Man Utd kuibomoa Southampton
Shughuli za Bandari zimeongezeka: Mrisho