Klabu za Manchester United na Liverpool zinatarajia kuingia katika vita ya kuiwania saini ya Beki kutoka nchini Senegal na Klabu ya Barcelona Mikayil Ngor “Mika” Faye.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 anadaiwa kusakwa sana na klabu hizo za England, kufuatia kuonesha kiwango cha hali ya juu akiwa na kikosi cha Barcelona B, msimu huu 2023/24.

Taarifa zilizochapishwa kwenye Gazeti la The Sun la England zinadai kuwa, Manchester United imedhamiria kupambana katika vita hiyo, huku ikifahamu wazi mpinzani wake Liverpool ana mpango wa usajili wa Kinda huyo.

Mashetani Wekundu wanaripotiwa kuwa katika nafasi nzuri ya kumsajili Faye, ambaye tayari imedhihirika ana kiu ya kucheza soka lake nchini England.

Taarifa nyingine kuhusu kinda huyo zilizochapishwa na Gazeti la Mundo Deportivo la Hispania zinadai kuwa, Liverpool inajipanga kuipiku Manchester United, katika mpango wa kuwasilisha ofa nono huko Camp Nou.

Hiyo ni kulingana na Uongozi wa Liverpool kushinikizwa na Benchi lao la Ufundi kufanikisha mpango wa kumsajili kijana huyo wakati wa usajili wa majira ya kiangazi.

Walimu wa Sayansi kuboreshewa maslahi
Mtemvu aibana Serikali utekelezaji miradi ya Maji Kibamba