Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kushirikiana na Wadau wamekubaliana kuunganisha nguvu katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, ili kuikamilisha kwa wakati na viwango stahiki.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, Oswald Urassa amesema wakubaliana kila Mkandarasi kuandaa na kuwasilisha mpango mkakati wake na jinsi atakavyotekeleza kazi na kukamilisha mradi kwa wakati.
Amesema, “Fedha hizi ni za wananchi hivyo ni lazima zitumike kama inavyopaswa. Hivyo, ni jukumu lenu ninyi Wakandarasi kuhakikisha mnatimiza makubaliano yetu tuliyoazimia leo ya kukamilisha miradi kwa wakati.”
Makubaliano hayo, yamefikiwa katika kikao kazi kilichojumuisha Ujumbe kutoka REA ukiongozwa na Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, Oswald Urassa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Ngusa Samike, Ujumbe kutoka TANESCO, Wabunge wa Lindi pamoja na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani humo.