Shirika la ndege la Precision Air limetoa Tsh. milioni 20 kwa Vikundi vya Wavuvi na mahitaji muhimu kwa vituo vitano vilivyopo Bukoba huku Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Patrick Mwanri akisema wameamua kufanya hivyo ikiwa ni ishara ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu pamoja na Wakazi wa Bukoba kwa kuwakimbilia wakati wa ajali ya PW 494.
“Hatuna budi kusema Asante kwa namna Mwenyezi Mungu ameendelea kutupatia nguvu na ujasiri kwa wakati wote, kidogo hiki tunachotoa kinabeba shukrani zetu za dhati, ushujaa uliooneshwa na Wavuvi waliokuwa karibu na eneo la tukio hauwezi kulipwa kwa thamani yeyote ila nawaomba mpokee mchango huu kidogo kama ishara ya kutambua juhudi zenu”
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mjini Erasto Sima amewapongeza Precision Air kwa kufanya jambo la kiungwana na kuwataka kuendelea na moyo huo wa kuwakumbuka wenye mahitaji na kuwatoa hofu Wananchi na kuwataka kuendelea kusafiri na Precision Air kwani ni salama na kwamba ajali iliyotokea inaweza kutokea kwa shirika lolote Duniani.