Wadau wa tasnia ya Habari, wamesema sheria zinazosimamia vyombo vya habari Zanzibar zinahitaji kufanyiwa marekebisho, kutokana na baadhi ya vifungu vyake kukandamiza uhuru wa habari.
Wakizungumza katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa TAMWA ZNZ wamesema miongoni mwa sheria ambazo zina mapungufu ni ile ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988.
Wamesema, sheria hiyo iliyofanyiwa marekebisho na sheria Na.8 ya mwaka 1997, sheria ya Tume ya Utangazaji ya Zanzibar Na. 7 ya mwaka 1997 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010 pamoja na sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015.
Nyingine ni sheria ya kufuta sheria ya Baraza la Wawakilishi (kinga, uwezo na fursa) namba. 4 ya 2007 na kutunga sheria mpya ya Baraza la Wawakilishi (kinga, uwezo na fursa) katika kutekeleza kazi na mambo mengine yanayohusiana na hayo Na. 6 ya 2022.
“Sheria ya kufuta Sheria ya Uchaguzi namba. 11 ya 1984 na kutunga sheria ya uchaguzi ya mwaka 2017 na masuala mengine yanayohusiana nayo pamoja na sheria ya kufuta sheria ya adhabu Na. 6 ya 2004 na kutunga sheria mpya ya adhabu, kuweka masharti bora zaidi pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo,” wamesema.
Awali, akiwasilisha mapitio ya sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria Na. 8 ya mwaka 1997 mkufunzi wa habari, Imane Duwe alisema Kifungu cha 3 cha sheria hiyo kimempa Waziri mamlaka ya kuteua Msajili wa Vitabu na Magazeti lakini iko kimya juu ya sifa na uzoefu wa msajili huyo.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa aliwataka waandishi wa habari kuendelea kufanya ushawishi wa mabadiliko ya sheria zenye mapungufu ili kutoa fursa ya upatikanaji wa sheria zinazoweka mazingira bora kwa vyombo vya habari Zanzibar kutekeleza majukumu yake.
TAMWA Zanzibar, shirika la Internews Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari wanaendelea kuangalia mapungufu yaliyopo katika sheria zinazosimamia sekta ya habari Zanzibar, ili ziweze kufanyiwa marekibisho kwa lengo la kuweka mazingira rafiki ya vyombo vya habari kutekeleza majukumu yake kwa uhuru.