Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya shilingi trilioni 1.15 kwa mwezi Oktoba ikiwa ni kukamilisha malengo waliyojiwekea katika ukusanyaji wa mapato.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi  Richard Kayombo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dar es salaam kuhusu  hali ya makusanyo na zoezi la uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN) linaloendelea kufanyika.

“Tumefanikiwa kukusanya shilingi Trilioni 1.15 kwa mwezi Oktoba mwaka huu ikiwa ni kufanikisha malengo ya ukusanyaji kodi nchini ili kukuza uchumi wa nchi pamoja kusaidia Serikali kuendeleza huduma za jamii nchini” alisema  Kayombo.

Katika hatua nyingine TRA imefanikiwa kushinda kesi 9 kati ya 10 zilizokuwa zikiendelea katika mahakama mbalimbali nchini dhidi ya walipa kodi wake na kufanikiwa kupata kiasi cha takribani Bilioni 16.9 .

Hata hivyo, Kayombo amesema kuwa zoezi la uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipa kodi ambalo limeanza hivi karibuni linaendelea na litafikia tamati Novemba 30 mwaka huu kwa mkoa Dar es salaam hivyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya uhakiki huo.

Tambwe, Mavugo Watemwa Intamba Mu Rugamba
Jaji Mutungi avifutia usajili vyama vitatu vya siasa