Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ukarabati wa meli ya MV Umoja kutarudisha huduma ya usafirishaji wa mizigo katika kanda ya ziwa kupitia bandari ya Kemondo iliyopo mkoani Kagera.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua Bandari hiyo kuangalia maendeleo yake.
Prof. Mbarawa ameitaka TRL kukarabati njia za reli bandarini hapo haraka iwezekanavyo ili kuruhusu mizigo itakayokuja ikiwa kwenye mabehewa kwa njia ya meli iweze kupakuliwa pindi Meli hiyo itaposhusha.
“Serikali imefanya ukarabati wa meli ya MV Umoja ambayo itabeba mizigo ikiwa kwenye mabehewa na reli hii inahitaji ukarabati mapema ipasavyo nawaagiza TRL kufanya ukarabati wa reli ili kusiwepo usumbufu wowote wakati wa kushusha na kupakia mizigo hiyo” , amesema Profesa Mbarawa.
Aidha, ameiagiza Mamlaka hiyo kuanza kutafuta wateja ambao kwa muda mrefu walikuwa wamepotea kutokana na bandari hiyo kusuasua kutoa huduma zake kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Meneja wa TPA Kanda ya Ziwa, Abel Moyo, amemuahidi Waziri huyo kutekeleza agizo lake kwa kushirikiana na TRL pamoja na MSCL na kuwahakikishia wafanyabiashara wa kanda ya ziwa kuwa na matumaini mpya ya kupata usafiri bora na wa uhakika.
Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoani humo Eng. Zephrine Bahyona, amezitaja baadhi ya changamoto zinazoathiri utendaji mzuri wa kivuko hicho kuwa ni kukatika kwa magugu maji na hivyo kupelekea kusombwa kwa kivuko.