Safari ya meneje wa Arsenal Arsene Wenger, kuondoka Emirates Stadium huenda ikatimia mwishoni mwa msimu huu, endapo atashindwa kuheshimu maamuzi ya bodi ya klabu hiyo ya kumuajiri mkurugenzi wa michezo ambaye atakua na kauli ya mwisho kuhusu mambo ya usajili na mambo mengine ya maendeleo ya kikosi.
Wenger tayari ameshaonyesha kukataa uamuzi huo wa viongozi wa juu wa Arsenal kwa kusema hatokubali kuona klabu hiyo inamuajiri mtu ambaye atakua juu yake.
Meneja huyo kutoka nchini Ufaransa, amewaambia waandishi wa habari kuwa atakataa kufanya kazi na mkurugenzi wa soka na anataka madaraka kamili juu ya benchi la ufundi.
Nafasi ya ukurugenzi wa michezo haijawahi kuwepo tangu meneja huyo alipoanza kazi mwaka 1996.
Lakini Wenger ambaye mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu huu, akasema: “Sielewi kabisa mkurugenzi wa ufundi ana kazi gani.
“Je ni mtu anayesimama barababarini na kuelekeza cheza kushoto na kulia? Sielewi kabisa na siwezi kuelewa majukumu yake.
“Mimi ni meneja wa klabu ya Arsenal na kadri nitakavyoendelea kuwa meneja, nitakuwa na kauli ya mwisho juu ya mambo yote ya soka ikiwemo benchi la ufundi.
“Baadhi ya makocha wanapendelea kuwa na jukumu moja tu, la kufundisha timu, na wanafurahia hilo. Mimi si aina ya watu hao”. Amesema Wenger