Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi kwamba ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli katika maeneo mbalimbali nchini zitakuwa zimetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90 ifikapo mwaka 2020.
Ameyasema hayo alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kituo cha Polisi cha Tarakea wilayani Rombo, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwahudumia wananchi na kuhakikisha huduma mbalimbali za kijamii kama maji, afya, nishati, elimu na miundombinu zinapatikana kwa uhakika.
Waziri Mkuu amewataka wananchi waendelee kuwa na Serikali yao ambayo imejipanga kutekeleza ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. Magufuli kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 inavyoelekeza.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amewatahadharisha watumishi wazembe, wezi, wala rushwa na waiowajibika hawana nafasi katika Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watumishi wote waimarishe utendaji wao.
“Iwapo watumishi wa umma watatimiza majukumu yao ipasavyo changamoto nyingi zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji zitakuwa historia kwa kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.”
Hata hivyo, Majaliwa ameongeza kuwa kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, ambapo itahakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma ya maji karibu na makazi yao.