Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora – THBUB, imekamilisha uchunguzi iliyouanzisha yenyewe kwa mujibu wa Kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria yake, Sura ya 391, kinachoipa uwezo wa kuanzisha uchunguzi ambao umeonesha kuwa kifo cha Mwanafunzi wa UDOM, Nusura Hassan Abdallah hakihusiani na ajali ya Dkt. Festo Dugange.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dodoma Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu amesema Katika uchunguzi huo THBUB ilitembelea eneo ilipotokea ajali ya gari iliyomhusisha Dkt. Dugange; nyumbani kwa Dkt. Dugange; Kituo cha Polisi (Traffic) Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Benjamin Mkapa, na Chuo Kikuu cha Dodoma.
Amesema pia ilitembelea Kijiji cha Mandewa, Kata ya Mandewa, Wilaya ya Singida Mjini wanakoishi wazazi wa marehemu Nusura Hassan Abdallah; Kitongoji cha Mtakuja Kijiji cha Kikonge, Wilaya ya Iramba alikozikwa Nusura; Ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro; Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, Mkoa wa Kilimanjaro; na maeneo mengine kwa madhumuni ya kupata maelezo ya watu mbalimbali kuhusu ajali ya Naibu Waziri na mazingira ya kifo cha Nusura Hassan Abdallah.
Amesema baada ya kupata maelezo katika maeneo yote ilikofika, THBUB imebaini usiku wa tarehe 25 Aprili, 2023 kuamkia tarehe 26 Aprili, 2023 ilitokea ajali ya gari maeneo ya Iyumbu, karibu na Njia Panda ya Shule ya Mfano, Jijini Dodoma ambapo gari iliacha njia, kugonga mti na kupinduka, na baada ya kupata majeraha kutokana na ajali hiyo, Dkt. Dugange alihangaika kutafuta msaada ili aweze kufikishwa hospitali kupata matibabu. Majira ya alfajiri ya tarehe 26 Aprili 2023, Dkt. Dugange alipata msaada wa boda boda iliyomfikisha Hospitali ya Benjamin Mkapa
Tarehe 27 Aprili, 2023, Marehemu Nusura Hassan Abdallah aliyekuwa Mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dodoma alisafiri kuelekea Moshi mkoani Kilimanjaro kwa basi la Manning Nice baada ya gari la Kapricon alilokuwa amepanga kusafiria kuchelewa, Basi hilo la Manning Nice lilimfikisha Babati na baadaye kupanda gari aina ya Coaster mpaka Arusha na kumalizia safari yake hadi Moshi kwa basi la Ibra Line”, amesema
Marehemu Nusura Hassan Abdallah alipokelewa na mchumba wake Juma Mohamed Kundya, Mjini Moshi ambapo walifika nyumbani kwake saa tano usiku wa tarehe 27 Aprili, 2023.
“Lengo la safari hiyo lilikuwa ni kuzungumzia masuala ya uchumba wao na kupanga siku ya mchumba wake kwenda kujitambulisha nyumbani kwao Singida”, Amesema Mwaimu
Mara ya mwisho Marehemu kuwasiliana na familia yake ilikuwa tarehe 29 Aprili, 2023 na mara ya mwisho kuwasiliana na rafiki yake aliyekuwa akisoma naye Chuo Kikuu cha Dodoma ilikuwa tarehe 1 Mei, 2023 akiwa mzima wa afya.
Hata hivyo Mwaimu amesema tarehe 01 Mei, 2023, Marehemu Nusura aliandaa chakula cha jioni ambacho alikula yeye, mchumba wake na mpwa wa mchumba wake.
“Baada ya kumaliza kula, Marehemu Nusura alijisikia vibaya na kuanza kutapika hadi kuishiwa nguvu hali iliyosababisha kufikishwa Hospitali ya Faraja kwa matibabu. Pamoja na hatua mbalimbali za kitabibu zilizochukuliwa na Madaktari wa Hospitali hiyo, Nusura Hassan Abdallah alifariki dunia majira ya saa 5:00 usiku ya tarehe 01 Mei, 2023”, amesema
Vipimo vilivyofanywa na Hospitali hiyo vilionesha kuwa kifo cha Nusura Hassan Abdallah kilitokana na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu.
Daktari aliyempatia huduma na ndugu wa marehemu walioutayarisha mwili kwa ajili ya mazishi na kuuona mwili huo kabla ya mazishi walithibitisha kuwa haukuwa na dalili za kupigwa, kujeruhiwa wala majeraha.
Mwaimu ameongezea kwa kusema Kutokana na mazingira hayo, THBUB imebaini kuwa kifo cha Marehemu Nussura Hassan Abdallah hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya gari aina ya Toyota Land Cruiser GXR V8 yenye namba za usajili T454 DWV iliyomhusisha Mhe. Dkt. Festo John Dugange, Naibu Waziri TAMISEMI (Afya) iliyotokea usiku wa tarehe 25 kuamkia tarehe 26 Aprili, 2023 katika eneo la Iyumbu, jijini Dodoma.
“THBUB haikuweza kuthibitisha mtu yeyote kuhusika na kifo cha Marehemu Nusura Hassan Abdallah kutokana na vielelezo vya Hospitali ya Faraja, Mkemia Mkuu wa Serikali, na maelezo ya mengine ya mashahidi” , amesema Mwaimu.