Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila amewataja watu 19, walipoteza maisha kwenye ajali hiyo sambamba na manusura ambapo ameeleza kuwa hali zao zinaendelea vizuri huku safari za Ndege mjini Bukoba zikisitishwa kwa muda usiojulikana.
Waziri Mkuu amesitisha shughuli zote za ndege katika uwanja huo, huku Mkuu wa Mkoa wa Kagera akiwataja marehemu hao kuwa ni kuwa ni Neema Faraja, Hanifa Hamza, Aneth Kaaya, Victoria Laurean, Said Malat Lyangana, Iman Paul, Faraji Yusuph, na Lin Zhang.
Wengine ni Sauli Epimark, Zacharia Mlacha, Eunice Ndirangu, Mtani Njegere, Zaituni Shillah, Dk Alice Simwinga, Afisa wa kwanza wa ndege hiyo, Peter Odhiambo ndugu wa familia moja Atulinde Biteya na Aneth Biteya, wakiwa miongoni mwa watu 43 waliokuwa kwenye ndege ya Precision Air.
Ndege hiyo, ilipata ajali Jumapili (Novemba 6, 2022), asubuhi ikitokea Mkoani Dar es Salaam kwenda Mwanza kupitia Bukoba baada ya kuanguka mita 100 kabla ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba mjini Mkoani Kagera.
Rubani wa ndege hiyo, Burundi Lubaga ambaye amekuwa nahodha wa ndege kwa karibu miongo miwili pia alifariki na hakuna miili mingine iliyopatikana huku taarifa za awali zikieleza kuwa ajali hiyo ilitokana na hali mbaya ya hewa.
Shirika la ndege la Air Tanzania likisitisha safari zake Jumapili kuelekea Bukoba na timu ya wataalamu kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa sasa ipo mjini Bukoba kuchunguza tukio hilo ambalo limeacha simanzi na majonzi kwa familia za marehemu na Watanzania kiujumla.
Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wote wametuma salamu zao za faraja kwa familia za waathirika wa ajali hiyo.