Watu zaidi ya 100 wamefariki dunia katika ajali ya ndege aina ya Boeing 737, iliyoanguka karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jose Marti, Havana nchini Cuba.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya umma nchini humo, watu watatu wamenusurika katika ajali hiyo mbaya iliyotokea jana.
Shirika la Mexico ambalo lilikodisha ndege hiyo limeeleza kuwa kulikuwa na abiria 110 pamoja na wafanyakazi wa ndege hiyo.
Serikali ya Cuba imetangaza siku mbili za maombolezo kufuatia ajali hiyo ambayo ni mbaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya nchi hiyo tangu miaka ya 1980. Ndege hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kuruka ikitokea Havana kwenda Holguin, mashariki mwa kisiwa hicho.
Kulikuwa na wafanyakazi sita wa ndege ambao ni raia wa Mexico, abiria wengi walikuwa raia wa Cuba pamoja na abiria watano ambao ni raia wa kigeni, kwa mujibu wa mtandao unaoratibiwa na Serikali ya Cuba uitwao ‘cuberdebate’.
Rais wa Cuba, Miguel Diaz-Canel ametembelea eneo la ajali hiyo na kusema, “imetokea ajali ya anga ya bahati mbaya. Habari hii haitoi ahadi nzuri, inaonekana kuna idadi kubwa ya waliothiriwa.”
Ndege hiyo ilikuwa imekodishwa na Shirika la Ndege la Cuba, Cubana de Aviación kutka kwa kampuni ya Mexico inayojulikana kama Aerolineas Damojh.