Mshambuliaji Alexis Sanchez amerejea kwenye mazoezi ya kikosi cha timu ya taifa ya Chile na huenda akacheza mchezo wa keshokutwa wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 dhidi ya Uruguay.

Sanchez alizusha hofu katika kambi ya timu ya taifa ya Chile pamoja na kwenye klabu yake ya Arsenal, kufuatia jeraha la kiazi cha mguu alilolipata juma lililopita, hali ambayo ilimfanya akose mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Colombia.

Taarifa za kurejea mazoezini kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 huenda zikapokelewa tofauti na meneja wa Arsenal Arsene Wenger, ambaye alionyesha kushtushwa na taarifa za kuumia kwa Sanchez.

Wenger anahofia kumkosa Sanchez kwa muda mrefu endapo itatokea anatonesha majeraha yake, hali ambayo huenda ikaathiri kasi ya kikosi chake cha Arsenal ambacho kinakabiliwa na michezo ya ligi ya nchini England pamoja na ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Mzee huyo kutoka nchini Ufaransa alimtahadharisha kocha mkuu wa timu ya taifa ya Chile Juan Antonio Pizzi kutoharakisha kumtumia Sanchez na badala yake alimuomba amrejeshe jijini London ili afanyiwe vipimo chini ya uangalizi wa matabibu wa Arsenal.

Tahadhari iliyotolewa na Wenger ilikuja, baada ya Pizzi kuwahakikishia waandishi wa habari mwishoni mwa juma lililopita kuhusu afya ya mashambuliaji huyo, ambapo alisema Sanchez huenda akacheza dhidi ya Uruguay.

Msimu uliopita Sanchez aliigharimu Arsenal baada ya kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya mwezi mmoja, kufuatia majeraha ya nyama za paja, na Arsene Wenger anaamini hali hiyo ilichangia kikosi chake kushindwa kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa England.

Trump: Wahamiaji haramu jiandaeni kuondoka
ACT-Wazalendo wahoji matumizi ya mabilioni ya Msaada wa Tetemeko