Hatma ya Tanzania katika mbio za kuwania tiketi ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani Gabon inatarajiwa kujulikana leo.

Tanzania, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inamenyana na Misri Saa 10:00 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Kundi G kufuzu AFCON.

Katika mchezo huo, Stars inahitaji ushindi tu ili kufufua matumaini ya kwenda AFCON ya mwakani, kwani sasa inashika mkia katika Kundi G, baada ya kucheza mechi mbili, ikifungwa moja ugenini na Misri 3-0 na kutoa sare moja ya 0-0 na Nigeria nyumbani.

Misri inaongoza kundi hilo kwa pointi zake saba baada ya kucheza mechi tatu sawa na Nigeria yenye pointi mbili.

Zote, Misri na Nigeria zimebakiza mchezo mmoja mmoja, wakati Tanzania ina mechi mbili – kwanza Jumamosi na Misri nyumbani na baadaye Septemba na Nigeria ugenini.

Iwapo Tanzania itashinda mechi zote mbili za mwisho watamaliza na pointi saba sawa na Misri, hivyo timu ya kufuzu AFCON ya mwakani kutoka Kundi G kupatikana kwa wastani wa mabao.

Mungu ibariki Tanzania. Ibariki Taifa Stars. Amin.

Ray Leonard, MIke Tyson Watoa Heshima Zao Za Mwisho
Zlatan Ibrahimovic Kusajiliwa Kabla Ya Euro 2016