Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaasa Watanzania kutambua kuwa utulivu, amani, umoja na mshikamano ndiyo nguzo muhimu katika ustawi wa Taifa kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Majaliwa ametoa wito huo wakati akizungumza na washiriki wa Kongamano la Mafunzo ya Shirikisho la Kimataifa la Polisi Wanawake – IAWP, Kanda ya Afrika lililofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Akimuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa kongamano hilo, amesema: “Uhuru huu wa mawazo tuliyonayo unatolewa kikatiba na pia unaenda na wajibu. Watu wasisahau kuwa umoja wa nchi umejengwa siku nyingi, tusitamani kuuharibu kwa manufaa ya wachache.”

Aidha, amewataka washiriki wa kongamano hilo, kuwa chachu ya mabadiliko katika utendaji kazi na mfano kupitia maarifa mapya watakayoyapata na kuwashirikisha ambao hawajapata fursa ya kushiriki katika mafunzo hayo.

Kuhusu umuhimu wa mafunzo, Waziri Mkuu amesema: “Askari wa kike, changamkieni fursa za mafunzo ya taaluma adimu ndani ya Jeshi la Polisi, na hii ni namna bora ya kuongeza uwakilishi wa wanawake katika kila idara ndani ya jeshi.”

Katika kongamano hilo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitunukiwa tuzo maalum kwa kutambua na kuthamini mchango wa askari wa kike nchini na kuwaamini kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

Nchi iendeshwe kwa kuzingatia mahitaji ya Wananchi - Othman
Vijana acheni kuuza figo - Dkt. Mpango