Mtuhumiwa wa mauaji ya kikatili ya mwanamke aliyekuwa akiishi naye kama mkewe Wilayani Moshi, amemtumia ujumbe mama mkwe akieleza mazingira ya mauaji hayo.

Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro linamsaka mtuhumiwa huyo baada ya kukuta mwili wa Josephine Mngara mwenye umri wa miaka 27, ukiwa umeteketezwa kwa moto kwenye jumba ambalo ujenzi wake haujamalizika, Februari 19, 2023. Aidha, polisi walieleza kuwa walikuta michirizi ya damu kutoka kwenye nyumba aliyokuwa anakaa mtuhumiwa kuelekea kwenye jumba hilo.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wakati jeshi la polisi likiendelea na msako, Mama Mzazi wa marehemu, Theodora Msuya ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa ametumiwa ujumbe mfupi was imu na mkwewe huyo, ambaye ameeleza kwa ufupi, akidai kuwa moyo wake unamuuma.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, ujumbe uliotumwa na mama mkwe, unasomeka kama walivyouhariri kwa kuficha jina lililotajwa, “mama samahani si kosa langu, nilimkuta (anamtaja) na mke wangu kwangu, nikavunja mlango tukaanza kupigana. Mimi nikashika panga na yeye akachukua mpini wa jembe. Akawa anarusha nikakwepa ndo akampiga mke wangu mpaka chini. Akanipa nauli akaniambia sepa niachie mimi… Muulize (anamtaja), mama mimi sijui roho yangu inauma sana mchana mwema.”

Mama huyo ameliomba jeshi la polisi kuwapa familia mabaki ya mwili wa mtoto wao ili wamfanyie maziko. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamewasilisha vinasaba (DNA) kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi.

Taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani humo ilieleza kuwa uchunguzi wa awali ulibaini chanzo cha kifo cha Josephine ni wivu wa mapenzi.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori amesema mwili wa marehemu unahifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), kwa ajili ya uchunguzi zaidi.  

Zitto Kambwe aikaba TFF, Young Africans
Kipindupindu chapungua Afrika, mafuriko kuongeza hatari