Mama Anne Kilango Malecela ambaye jana alitengeneza habari kubwa kila kona baada ya Rais John Magufuli kutangaza kutengua uteuzi wake kama Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, amesema jambo kuhusu taarifa hizo.

Jana, Rais Magufuli alieleza kusikitishwa kwake na taarifa zilizotolewa na Anne Kilango kuwa hakukuwa na Mfanyakazi hewa katika Mkoa wake ili hali timu ya Ikulu ilibaini uwepo wa wafanyakazi hewa 45 katika awamu ya kwanza ya uchunguzi wao.

Rais Magufuli alieleza kuwa alijiuliza maswali mengi kabla ya kufanya uamuzi wa kumuondoa mwanasiasa huyo mkongwe aliyekuwa akitikisa Bungeni, lakini pia alimuondoa Katibu Tawala wa Mkoa huo ambaye alimshauri vibaya Mama Malecela.

Kipindi cha Sun Rise cha 100.5 Times Fm iliyoko jijini Dar es Salaam kimezungumza kwa njia ya simu na Mama Anne Kilango lakini alibainisha kuwa hakuwa na taarifa rasmi za uamuzi huo wa Rais.

“Jamani mimi sina taarifa,” alisema Mama Malecela. “Sipendi kuzungumzia jambo hilo maana sijaambiwa na aliyeniteua, sina la kukwambia,” aliongeza kabla ya kukata simu.

Mama Anna Kilango alikuwa Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika Serikali ya Awamu ya Tano.

 

Marcelo Bielsa Kupambanishwa Na Brendan Rodgers Swansea City
597 Waliofutwa kazi NIDA kupata 'chao'