Mahakama ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe imempandisha kizimbani, Babu Enock mwenye umri wa miaka 35, kwa shtaka la kutumia vyeti vya mtu mwingine kuanzia mwaka 2015-2019.
Babu anatuhumiwa kuisababishia hasara serikali ya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 28 ambazo alilipwa mshahara na TAMISEMI, kwa kutumia cheti cha Silvano Emanuel Minchi.
Akisoma mashtaka hayo mwendesha mashtaka wa Jamhuri Leonard Chacha, mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa Wilaya ya Momba, Zabibu Mpangule amesema kuwa mshtakiwa huyo anashtakiwa kwa makosa matatu kosa la kwanza ni wizi kinyume na kifungu cha sheria 265 kanuni ya adhabu sura ya 16, kosa la pili kuisababishia hasara serikali kinyume na kifungu cha sheria 28 A kanuni ya adhabu sura ya 16, na kosa la tatu uhujumu uchumi kinyume na kifungu cha sheria 57 na 60 kanuni ya adhabu sura ya 16.
Aidha mwendesha mashtaka Chacha ameongeza kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka la wizi wa cheti cha elimu ya sekondari CSMO 043657 chenye jina la Silvano Emanuel na kutumia cheti hicho kujipatia fedha.
Kwa upande wake mshitakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwasababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na amerudishwa rumande kwa kukosa dhamana mpaka kibali kitapopatikana kutoka kwa mkaguzi wa mashtaka.