Mabingwa wa soka Afrika mashariki na kati Azam FC, wametangaza kuachana na mshambuliaji kutoka nchini Ghana, Yahaya Mohammed.
Azam FC wamefikia hatua hiyo baada ya kuona Yahaya Mohammed ameshindwa kuonyesha kile walichokitarajia, hivyo kuamua kumpa nafasi kuondoka huku wakiahidi kuijaza nafasi yake kupitia dirisha dogo la usajili ambalolitafunguliwa siku za karibuni.
Hata hivyo inahisiwa huenda maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia kauli iliyowahi kutolewa na Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioba kupitia vyombo vya habari, ambapo alieleza anahitaji washambuliaji wengine wawili ili kuongeza nguvu ya kikosi chake.
“Nichukue nafasi hii kuwafahamisha kwamba hatutaendelea kuwa naye, uongozi umekutana naye, wamezungumza kuhusiana na suala lake na wamemalizana. Hivi sasa Mohamed sio mchezaji tena wa Azam FC baada ya makubaliano kati yake na uongozi,” alisema Jaffary Idd, Msemaji wa Azam FC.
Maganga amesema tayari wameshampatia release letter na pamoja na hayo tayari wameshampatia kila kitu ikiwemo tiketi ya ndege ambapo wanatarajia ataondoka kurudi kwao Ghana Jumanne hii.
“Tutamkumbuka Yahaya, kwa Maana kwamba yale ambayo ameyafanya kwenye timu yetu, ametusaidia kupata ubingwa wa Kombe la Mapinduzi na pia msimu ndiye aliyefunga bao la kwanza,” amesema.
Mbadala wa Yahaya Mohamed kwa mujibu wa Afisa Habari Jaffary Maganga, ni kwamba atatangazwa baada ya benchi la ufundi kufanya tasmini na kuchambua wale wanaowahitaji.
Mshambuliaji huyo alijiunga na Azam akitokea Aduana Stars ya Ghana, ambayo aliisaidia kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Ghana msimu 2015/16, Mohammed pia aliiibuka mfungaji bora namba mbili wa ligi hiyo kwa mabao 15 aliyofunga nyuma ya Latif Blessing wa Liberty Proffesional aliyetupia 17.
Mohammed alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ghana kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zilizofanyika mwaka juzi nchini Afrika Kusini na timu hiyo kuwa washindi wa pili.
Wakati anaanza, alionyesha cheche zake lakini baadaye alionekana kushindwa kufanya vema kama ambavyo wengi walitarajia afanye.