Wakati siku zikiendelea kusogea kabla ya mchezo wa mzunguuko wa tatu hatua ya mtoano wa ligi ya mabingwa barani Afrika, kati ya Young Africans dhidi ya Al Ahly, kocha mkuu wa mabingwa wa soka Tanzania bara, Hans Van der Pluijm amesema kikosi chake kina kazi ngumu katika mchezo huo ambao utapigwa jijini Dar es salaam mwishoni mwa juma lijalo.

Pluijm, amesema kikosi cha Al Ahly watakachokutana nacho katika mchezo wa hapa nyumbani pamoja na ule wa ugenini, kina uwezo mkubwa wa kiushindani, hivyo hana namna ya kujipanga vyema na kubuni mbinu mbadala za kukikabili katika michezo yote miwili.

“Ni lazima tujiandae vilivyo, hautakuwa mchezo rahisi kwetu wala kwao, lakini sina budi kukitazama kikosi changu kwa hali zote kutokana na hitaji la kutaka kusonga mbele kwa kuhakikisha tunaanza vyema katika uwanja wa nyumbani kabla hatujakwenda mjini Cairo,” alisema kocha huyo kutoka nchini Uholanzi.

“Ndiyo maana utaona kila leo tunafanya mazoezi ya kujiandaa na mchezo huo, licha ya kukabiliwa na michezo mingine ya hapa Tanzania, lakini jukumu kubwa ni mpambano wetu dhidi ya Al Ahly.”

Young Africans itakutana na Al Ahly, baada ya kuiondosha APR kutoka nchini Rwanda kwa jumla ya mabao matatu kwa mawili na kabl ya hapo waliichapa Circle de Joachim kutoka nchini Mauritius jumla ya mabao matatu kwa sifuri.

Utafiti: Karibu Nusu ya wanawake wanaojiuza wana Virusi vya Ukimwi
Abracadabra Azitaja Arsenal, Chelsea Na West Han Utd