Gavana wa jimbo la mpakani la Niger, Kanali Hubert Yameogo amesema Jumla ya Abiria 10 waliokuwa wakisafiri na basi wameuawa kutokana na mlipuko uliosababishwa na bomu lililotegwa ardhini mashariki mwa Burkina Faso.
Gavana huyo amesema, “Mchana wa Desemba 25, 2022, basi dogo la usafiri wa umma lilikanya bomu kwenye barabara Fada N’Gourma-Kantchari, karibu na kijiji cha Bougui na kwa bahati mbaya mlipuko huo ulisababisha vifo vya abiria kumi na kujeruhi wengine watano, waliokimbizwa katika hospitali ya Fada N’Gourma, mji mkuu wa mkoa huo.”
Hata hivyo, amebainisha kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwa kuwa abiria wengine hawajulikani waliko huku chanzo kimoja cha usalama kikithibitisha kutokea shambulio hilo kwa kusema, “Basi lilikuwa limeondoka Matiakoali kuelekea Fada N’Gourma na Wahanga wengi wamefariki hasa Wanawake na watoto.”
Tangu mwaka wa 2015, Burkina Faso imeshuhudia vifo mara kwa mara vilivyosababishwa na mashambulizi ya wanajihadi yenye uhusiano na Islamic State na Al-Qaeda yanayolenga wanajeshi na raia ambayo yameua maelfu ya watu na kuwalazimu takriban watu milioni mbili kuyakimbia makazi yao.