Imeelezwa kuwa, usalama na afya katika sehemu za kazi ni jambo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele kuliko jambo lolote lile hususan katika maeneo ya migodi.
Hayo ameyabainisha Waziri wa Madini Doto Biteko katika ufunguzi wa Kikao Kazi cha kujadili masuala ya usalama, afya na baruti kilichofanyika leo Septemba 13, 2021 katika ukumbi wa Chuo cha Madini Dodoma.
Waziri Biteko amesema lengo la kikao kazi hicho ni kujadili namna bora ya kulinda usalama, afya na baruti ili mwisho wa siku Wizara na Taasisi zake ziweze kufikia lengo la kukusanya bilioni 650 iliyopangiwa na Serikali na kuwaacha watu wakiwa salama.
Waziri Biteko amesema zinapofanyika shughuli za uchimbaji madini lazima athari za mazingira zitokee, hivyo amewataka wakaguzi wa migodi kote nchini kuziona athari kabla hazijatokea ambapo amesema ajali yoyote inapotokea lazima viashiria viwe vimeshabainishwa na wakaguzi wa migodi kabla ya ajali kutokea.
“Bora tukose hela lakini watu wetu wawe salama, nendeni mkakague kwa uangalifu na uaminifu, na pia msikague kwenye taka sumu pekee kagueni kote ikiwemo migodi ya kati na migodi ya wachimbaji wadogo, tusiwe bize na masuala ya dharura, hakikisheni mnafatilia ili mjue aina ya uchimbaji salama,” amesisitiza Waziri Biteko.
Aidha, Waziri Biteko amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Dkt. Abdul Rahman Mwanga kuwa Kamishna wa Madini na kueleza kuwa, jambo zuri kuteuliwa mtu ambaye ametoka miongoni mwao.
“Rais wetu anataka kila Wizara na Taasisi za Serikali zijisimamie zenyewe, zifanye maamuzi yaliyo sahihi, ukiona Rais kateua kiongozi kutoka miongoni mwenu ujue mnaaminika asingeshindwa kuteua mtu kutoka mahali pengine, endeleeni kufanyakazi kwa uaminifu ili kufanikisha kukusanya maduhuli tuliyopangiwa na kukuza uchumi wa nchi yetu,” amesema Waziri Biteko.
Naye, Kaimu Mwenyekiti wa Tume ya Madini Janet Ruben, amempongeza Waziri Biteko kwa kukubali kuhudhuria kikao hicho na amemuahidi kwamba, atahakikisha maelekezo yote aliyoyatoa yanafanyiwa kazi ili mwisho wa siku lengo makusanyo ya bilioni 650 yafanikiwe na yaendane na usalama wa afya za watu.