Baraza la Michezo la Taifa ‘BMT’ limethibisha kuendelea vyema kwa maandalizi ya Safari ya Kikosi cha Timu ya taifa ya Wanawake Chini ya Umri wa Miaka 17 (Serengeti Girls), kuelekea England kwa ajili ya kuweka Kambi kujiandaa na fainali za Kombe la Dunia.

Serengeti Girls itashiriki Fainali hizo zitakazounguruma nchini India mwezi ujao, baada ya kufuzu ikitoka katika Bara la Afrika ambalo litawakilisha na timu tatu. Timu nyingine kutoka Bara la Afrika ni Morocco na Nigeria.

Katibu Mtendaji wa ‘BMT’, Neema Msitha, amesema mikakati ya safari hiyo inaenda vizuri na muda wowote juma lijalo timu hiyo itaelekea England kuanza Kambi.

Msitha amesema Serengeti Girls itaenda kuweka kambi katika Kituo cha Klabu ya Southampton na wanaamini ikiwa huko Benchi la Ufundi litapata nafasi ya kutekeleza kwa ukamilifu programu zake za mazoezi na hatimaye kwenda India wakiwa imara.

“Maandalizi ya safari ya timu hiyo yanaendelea vizuri, baadhi ya vitu ikiwamo taratibu za kuomba VISA zimeshafanyika. Tumedhamiria kuhakikisha Serengeti Girls inaimariika kwa wachezaji na Benchi la Ufundi kupata maandalizi mazuri kuelekea Fainali hizo za Kombe la Dunia,” amesema Msitha.

Ameongeza tayari Serikali imeshakutana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa lengo la kuhakikisha timu hiyo inapata mihezo ya Kirafiki ikiwa Uingereza.

“Timu itakaa Uingereza kwa muda wote na itaondoka nchini humo kuelekea India ikiwa ni siku tatu au nne kabla ya fainali kuanza kwa lengo la kwenda kuipeperusha bendera ya Tanzania,” Msitha ameongeza.

Serengeti Girls ilifuzu kushiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza ikiwa na Kocha Mkuu, Bakari Shime, baada ya kuwaondoa Eritrea, Burundi na Cameroon kwenye hatua za awali.

Farouk Shikalo akubali lawama za mashabiki
Rais Samia asikitishwa kifo cha Mkurugenzi Igunga