Mlinda Lango wa Mtibwa Sugar Farouk Shikalo amepokea kwa masikitiko lawama zinazoelekeza kwake, baada ya kikosi chao kukubali kupoteza mchezo dhidi ya Young Africans juzi Jumanne (Septemba 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Mtibwa Sugar ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa 3-0, na ulikua mchezo wao wa kwanza kupoteza msimu huu 2022/23, baada ya kuanza vizuri kwenye michezo mitatu ya mwanzo.

Shikalo ambaye aliwahi kuitumikia Young Africans, kisha KMC FC kabla ya kutimkia Mtibwa Sugar amesema amejihisi vibaya kutokana na Mashabiki wa soka kumnyooshea vidole na kumtaja kama sababu kuu ya timu yao kupoteza kwa mabao 3-0.

Mlinda Lango huyo kutoka Kenya amesema maneno yamekua mengi katika Mitandao ya Kijamii tangu juzi Jumanne (Septemba 13) amekua akiyaona mara kwa mara, lakini akasisitiza kuwa Mashabiki wa soka wana haki ya kulaumu kwa sababu wanaamini wanachokiamini.

“Maneno yamekua mengi eti nimeruhusu ya kizembe, ninaheshimu mitazamo ya watu kwa sababu wana haki ya kusema lolote wanaloliona likitokea uwanjani, ila nina uhakika ninaifanya kazi yangu kwa weledi mkubwa.”

“Ni kawaida Mchezeji kulaumiwa pale anapoonekana amecheza chini ya kiwango, lakini kwangu sidhani kama nilicheza chini ya kiwago na kuruhusu kirahisi mabao kama inavyodaiwa, hii si mara ya kwanza mimi kulaumiwa na Mashabiki, imenikuta mara nyingi na ndio maana ninasema ninaheshimu sana mitazamo ya mashabiki.”

Kuhusu bao la tatu la Young Africans lililofungwa na Kiungo Mshambuliaji kutoka Burkina Faso Stephen Aziz Ki, Shikalo amesema mpigaji alikua makini na alitumia udhaifu wa wachezaji wa Mtibwa Sugar waliokua wamerundikana katika eneo la lango lao dakika za lala salama.

“Niliumia, kwa sababu wakati anaupiga ule mpira tulikua wengi katika eneo la goli letu, unaweza kulaumu kwa kusema ulikua ni uzembe lakini haikuwa hivyo, ninampongeza mpigaji kwani alitumia udhaifu wetu kutuadhibu.” amesema Shikalo

Mlinzi Jeneza la Malkia Elizabeth aanguka ghafla
BMT: Mipango ya Serengeti Girls ipo safi