Wanafunzi watatu wa kike nchini Burundi wanakabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela kwa kuharibu picha ya Rais Pierre Nkurunziza kwa kuchora kwenye madaftari yao.
Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu (HRW) limeeleza kuwa wasichana hao walikamatwa wiki iliyopita na wanasubiri kufikishwa mahakamani Jumatatu ijayo kwa kosa la kumkashfu mkuu wa nchi.
Shirika hilo limeeleza kuwa vyombo vya dola pia liliwakamata wanafunzi wengine saba, lakini wanne waliachiwa huru ikiwa ni pamoja na mtoto mwenye umri wa miaka 13 ambaye pia aliachiwa mara moja.
Wasichana hao watatu ambao wana umri wa miaka 18 walikaa rumande katika siku zote za wikendi.
Mkurugenzi wa HRW wa Afrika ya Kati, Lewis Mudge ameeleza kuwa mmoja wa wazazi wa watoto hao alieleza kuwa familia yake inaogopa.
HRW imekosoa hatua hiyo na kuitaka Serikali kujikita zaidi katika kupambana na watu wanaovunja haki za binadamu badala ya kuwabana watoto wanaochora michoro hiyo.
Ripoti ya Shirika hilo imeeleza kuwa mwaka 2016, vyombo vya dola nchini humo viliwakamata wanafunzi nane wa shule ya sekondari kwa tuhuma za kumkashfu Rais baada ya kuchora michoro isiyofaa dhidi ya mkuu huyo wa nchi.
Nkurunziza alishinda kwa kishindo katika uchaguzi wa mwaka 2015 uliompa nafasi ya kuendelea kuongoza nchi hiyo kwa awamu ya tatu.