Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema kuwa vikosi vya serikali ya Burundi na wanachama wa chama tawala wamewapiga na kuwatisha wafuasi wa vyama vya upinzani, wanaopinga kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika Mei 17 mwaka huu.
Tangu Desemba 12 mwaka jana, wakati rais Pierre Nkurunzinza alipotangaza kufanyika kwa kura ya maoni, maafisa wa serikali na wanachama wa kundi la ‘Imbonerakure’ yaani wale ‘wanaoona kutoka mbali’ wametumia vitisho na ukandamizaji kuhakikisha kura zinaelekezwa kumfaidisha rais Nkurunzinza.
Aidha, kura hiyo itamuwezesha rais huyo wa Burundi ambaye tayari anatumikia muhula wenye utata kurefusha muda wa kuitawala nchi hiyo hadi mwaka 2034.
Hata hivyo, tangu mwaka 2015 wakati mgoggoro wa kisiasa ulipoanza nchini Burundi, baada ya rais Nkurunzinza kutangaza kuwania muhula mwingine, chombo huru cha habari nchini humo na mashirika yasio ya kiserikali vimefungiwa huku zaidi ya watu 397,000 wakiitoroka nchi hiyo.