Mkaguzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Maxwell Mtonga kutoka Malawi ameridhia mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya wenyeji, Young Africans na MC Alger ya Algeria uchezwe Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Aprili 8, mwaka huu baada ya marekebisho madogo aliyoelekeza.

Mtonga yupo Mwanza tangu mwishoni mwa juma lililopita akiongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi katika ukaguzi huo na ameagiza marekebisho madogo madogo.

Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba, Steven Shijja amesema watahakikisha wanafanya marekebisho hayo ndani ya muda kama walivyoelekezwa na mchezo huo utafanyika Mwanza bila shaka

Viongozi wa Young Africans wapo katika harakati za kufanikisha mpango wa kuuhamishia mchezo huo Mwanza kutoka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa matarajio ya kupata watazamaji wengi na pato kubwa.

Tayari mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya wenyeji Mbao FC na Simba SC ya Dar es Salaam uliokuwa ufanyike Aprili 8, mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba, umesogezwa mbele kwa siku mbili hadi Aprili, 10.

Lakini taarifa ya Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura jana ilisema kwamba hatua hiyo imechukuliwa ili kupisha shughuli za kijamii kwenye Uwanja huo zitakazoanza Aprili 1 hadi 9.

Young Africans imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Zanaco Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia ikitoka kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Magazeti ya Tanzania leo Machi 29, 2017
Video: Wauza Nyama Dar Walia Bei Kushuka